Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naibu kamishna wa haki za binadamu amelaani mashambulizi dhidi ya raia Somalia

Naibu kamishna wa haki za binadamu amelaani mashambulizi dhidi ya raia Somalia

Naibu kamishna mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Kyung-Wha Kang amelaani vikali mashambulizi dhidi ya raia nchini Somalia na kutoa wito wa juhudi madhubuti kumaliza miongo miwili ya vita nchini humo.

Wha Kang ametoa tamko hilo hii leo baada ya kuhitimisha ziara ya siku tatu nchini Kenya, Somalia na Puntland. Amesema baada ya siku hizo tatu ameelewa matatizo na matumaini ya watu wa Somalia na kuona haja ya kufanya juhudi zaidi za kuchangia kuleta amani ya kudumu kwa nchi hiyo.

Amesema pia amekuwa na mazungumzo ya kina na uongozi wa serikali ya mpito ya Somalia, jumuiya za kijamii, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wajumbe wa jumuiya ya kimataifa Somaliland, Puntland na Nairobi Kenya. Pia amepata fursa ya kuzungumza na baadhi ya waathirika waliokimbia vita Moghadishu hivi karibuni na wanahifadhiwa kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Hargeisa.

Amesema ni vigumu kuapa lugha ya kueleza jinsi anavyolaani mashambulizi la ukatili dhidi ya raia unaofanywa na kundi la wanamgambo wa Al Shabaab na makundi mengine yenye silaha ambayo yamesababisha mamilioni ya watu kukimbia na pia kushambulia vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM. Amesema ni lazima kutafutwe njia za kuweza kuwalinda raia wasio na hatia.