Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kiwango cha elimu Palestina chaghubikwa na matatizo

Kiwango cha elimu Palestina chaghubikwa na matatizo

Wizara ya elimu na elimu ya juu ya Palestina, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Palestina UNRWA wameonya kuwa kiwango cha elimu Palestina kimefikiwa hali isiyokubalika licha ya juhudi za serikali na jumuiya ya kimataifa.

Onyo hilo linasema leo hii zaidi ya watoto milioni moja wanaorejea shuleni kwenye eneo linalokaliwa la Palestina wakabiliwa na mwendo mrefu jambo ambalo linawafanya wengine kutohudhuria masomo. Katika Ukanda wa Gaza asilimia 82 ya shule zilizoharibiwa na makombora bado hazijakarabatiwa na hivyo kuongeza shinikizo kwenye mfumo wa elimu ambao tayari umelemewa.

Idadi ya walimu haitoshi na kuna upungufu wa madarasa 1000 jambo ambalo limesababisha mrundikano madarasani na kuchangia wanafunzi wengi kuwa katika hatari ya kutohudhuria masomo kabisa. Wanafunzi zaidi ya 10,000 leo hii wanaanza masomo kwenye mahema, au vibanda na shule nyingi za serikali hazina huduma muhimu kama maji na vyoo.