Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya kina mama wakati wa kujifua vimepungua:UM

Vifo vya kina mama wakati wa kujifua vimepungua:UM

Makadirio ya Umoja wa Mataifa yamebaini kuwa vifo vya kina mama wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua vimepungua duniani kote lakini bado kina mama 1000 wanakufa kila siku.

Takwimu zilizoko kwenye ripoti mpya iitwayo Mtazamo katika vifo vya kina mama zinaonyesha kuwa idadi ya wanawake wanaokufa kutokana na matatizo ya wakati wa ujauzito au kujifungua imemepungua kwa asilimia 34 kutoka makadirio ya kvifo 546,000 mwaka 1990 hadi 358,000 mwaka 2008.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo na shirika la afya duniani WHO kwa ushirikiano na shirika la kuhudumia watoto UNICEF, shirika la idadi ya watu UNFPA na Bank ya dunia inasema hatua zilizopigwa zinaonekana lakini idadi ya punguzo kwa mwaka bado iko chini ya nusu ya ile inayohitajika ili kufikia malengo ya maendeleo ya milenia, ambayo yanataka kupunguzwa kwa idadi ya vifo vya kina mama wakati wa kujifungua kwa asilimia 75 kati ya mwaka 1990 na 2015.

Kwa mujibu wa Mmkurugenzi mkuu wa WHO Bi Margaret Chan ingawa hatua imepigwa bado kila siku kina mama 1000 wanafariki dunia kutokana na matatizo wakati wa kujifungua, na kati ya hao 570 wanaishi katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara, 300 Asia Kusini na 5 katika nchi zilizoendelea.