Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TFG na jumuiya ya kimataifa watimize wajibu wao kwa amani ya Somalia:Ban

TFG na jumuiya ya kimataifa watimize wajibu wao kwa amani ya Somalia:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa serikali ya mpito ya Somalia kumaliza mivutano ya ndani inayokuwa pingamizi kwa mambo muhimu na kuitaka jumuiya ya kimataifa kutoa msaada wa kijeshi na kifedha unaohitajika kukabbiliana majeshi yenye itikadi kali.

Ban katika ripoti yake mpya kuhusu Somalia kwenye baraza la usalama amesema ni muhimu kwa serikali ya mpito TFG kuweka mfumo mzuri wa serikali ili kutoa huduma kwa watu wake, akitoa mfano wa mivutano inayoendelea baina ya bunge na baraza la mawaziri, na haja ya haraka ya kuhakikisha ulinzi, usalama na huduma muhimu katika nchi hiyo iliyoghubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa takribani miongo miwili sasa tangu kupinduliwa kwa serikali iliyokuwa imara.

Amesema ili serikali ya mpito iweze kushughulikia changamoto inazokabiliana nazo, hasa kuwa na uongozi imara na kudhibiti tisho la itikadi kali, Ban ameiomba jumuiya ya kimataifa kuingilia kati katika kutoa msaada wa kijeshi, fedha na usaidizi mwingine.

Amesema pengo lililopo la ufadhili wa Umoja wa Mataifa kwa zaodi ya wanajeshi 5000 wa kulinda amani wa muungano wa Afrika AMISOM linaendelea kuzorotesha utendaji na pengine kuwavunja moyo nchi ambazo wangeweza kuchangia vikosi ili kupambana na wanamgambo wa Al-shabab na makundi mengine ya wanamgambo nchini humo.