Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi dhidi ya mashambulio ya raia Darfur ni muhimu:UM

Uchunguzi dhidi ya mashambulio ya raia Darfur ni muhimu:UM

Mtaalamu wa kujitegemea wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Sudan Mohamed Chande Othman leo ametoa wito kwa serikali ya Sudan kufanya kwa haraka uchunguzi huru dhidi ya mashambulio ya raia Kaskazini mwa Darfur yaliyosababisha kuuawa kwa raia wengi Septemba pili.

Bwana Chande amesema tukio hilo lazima lichunguzwe kwa kina na wahusika wafikishwe mbele ya sheria. Pia ameitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea na juhudi za kuvisaidia vikosi vya pamoja vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID ili waweze kutoa ipasavyo ulinzi kwa raia kama inavyotakiwa na baraza la usalama.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa mpya zilizokusanywa katika siku kumi zilizopita zinathibitisha taarifa za awali za kwamba watu zaidi ya 37 wameuawa na zaidi ya 50 kujeruhiwa baada ya kundi la wanamgambo la Janjaweed kushambulia raia waliokuwa wamekusanyika sokoni kwenye kijiji cha Tabarat Kaskazini mwa Darfur.

Bwana Chande pia ameelezea hofu yake juu ya kundi la UNAMID lililotakiwa kwenda kutathimini hali katika eneo la tukio, awali lilizuiliwa na majeshi ya serikali ya Sudan na kundi la wanamgambo wenye silaha.