Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yaalani vikali mauaji dhidi ya waandishi habari

UNESCO yaalani vikali mauaji dhidi ya waandishi habari

Mkuu wa shirika la umoja wa mataifa linalohusika na masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO Irina Bokova amelaani mauaji ya waandishi wanne wa habari yaliyofanyika juma lililopita na kutoa wito kwa serikali kufanya kila njia kuwafikisha mahakamani wahusika.

Waliouawa ni pamoja na Sayed Hamid Noori raia wa Afghanistan, Alberto Graves Chakussanga raia wa Angola , safaa al- Khayat na Riad al-Saray wote raia wa Iraq kwenye mauaji yaliyofanyika kati ya tarehe tano na nane mwezi huu.

Kulingana na shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka, Noori mmoja wa waandishi hao ambaye pia hapo awali alikuwa msomaji maarufu wa habari wa kituo kimoja cha runinga nchini Afghanistan na ambaye hadi kifo chake alikuwa akihudmu kama msemaji wa spika la bunge alichomwa kisu na kuuawa tarehe tano mwezi huu mjini Kabul.

Bokova amesema kuwa kazi ya waandishi wa habari ni muhimu kwa haki ya kuzungumza akisema kuwa kuitetea haki hii ni muhimu kwa nchi kama Afghanistan na Iraq zilizokumbwa na mizozo.