Muhimu kwa nchi zinazoendelea kupata vifaa vya afya:WHO

Muhimu kwa nchi zinazoendelea kupata vifaa vya afya:WHO

Wataalamu wa afya zaidi ya 350 kutoka nchi zaidi ya 100 wanakutana leo katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na shirika la afya duniani WHO mjini Bankok Thailand.

Kongamano hilo ni la kutathimini ushahidi mpya na kukubaliana njia za kuimarisha uwezo wa kupata vifaa vya tiba vinavyoweza kuokoa maisha katika nchi zinazoendelea. Akizungumza katika kongamano hilo mkurugenzi mkuu wa WHO Bi Margareth Chan amesema sekta ya vifaa vya matibabu inatoa matumaini makubwa kwa afya ya jamii, na tena ni matumaini muhimu. Ameongeza kuwa maafisa wa afya na mameneja wa hospitali katika nchi zote , na katika viwango vyote vya maendeleo wanahitaji muongozo.

Na amesema wanafanya kongamano hili kwa sababu faida za vifaa vya matibabu haziwiani na ugawaji wake hauko sawia. Kwa mujibu wa WHO leo hii kuna vifaa takribani aina 10,500 vya matibabu kwenye soko la kimataifa, kuanzia vya gharama nafuu hadi vya bei kubwa na vinasaidia katika masuala mbalimbali.

Utafiti mpya wa WHO ulioitwa Medical Devices umebaini kuwa vifaa vya matibabu vinatumika katika nchi 140 duniani na watu wengi hawana fursa ya kuvipata hivyo mkutano unasema ni muhimu kuongeza uwezo wa kuweza kupatikana vifaa hivyo katika nchi zinazoendelea kutasaidia sana kuokoa maisha ya watu.