Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tafadhali Rwanda msiondoke Sudan:Ban

Tafadhali Rwanda msiondoke Sudan:Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani nchini Rwanda leo ameitaka nchi hiyo kutomaliza operesheni zake za kulinda amani nchini Sudan, katika jitihada za kujaribu kumaliza mvutano unaoshika kasi kuhusu ripoti ya Umoja wa Mataifa.

Ban amesema ripoti hiyo ambayo bado ni rasimu inasema wanajeshi wa Rwanda huenda wametekeleza mauaji ya kimbari nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wakati wa miaka 1990 na itatolewa baada ya wanachama wa Umoja wa Mataifa na wadau wengine kupata fursa ya kutoa maoni kuhusu ripoti hiyo.

Ban amesema ninaheshimu mchango wa Rwanda katika ajenda ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan, nimemuomba Rais Paul Kagame kuendelea na mchango wake kote duniani na hususan Sudan ambako tutashuhudia kura ya maoni Januari mwakani.

Ban aliwasili Rwanda jana Jumanne na ameondoka leo baada ya kukutana na Rais Kagame na waziri wa mambo ya nje wa Rwanda Louise Mushikikwabo. Rwanda inasema shutma katika ripoti hiyo sio za kweli na ni upuuzi, na kusisitiza kuwa itachukua hatua kali endapo ripoti hiyo haitofanyiwa marekebisho.