Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNHCR azuru makambi ya wakimbizi Kenya

Mkuu wa UNHCR azuru makambi ya wakimbizi Kenya

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR Antonio Guterres leo ameanza ziara ya siku tatu kwenye makambi ya wakimbizi wa Kisomali nchini Kenya.

Katika ziara hiyo bwana Guterres atatathmini mpango wa nishati inayojali mazingira katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini mashariki mwa Kenya na pia kutathimini hatua zilizopigwa katika upanuzi wa kambi iliyofurika ya Dadaab karibu na mpaka wa Somalia.

Kambini Kakuma bwana Guterres ataangalia mradi wa majaribio wenye lengo la kuwapa nishati ya umeme wakaazi wa kambi hiyo, shule, hospitali na huduma zingine za jamii, na wakati huohuo wakianzisha nishati ya jua nay a kutumia upepo.

Kesho Jumatano bwana Guterres atakuwa kambini Dadaab kuangalia upanuzi wa sehemu ya Ifo ya kambi hiyo ambapo ukikamilika utaruhusu wakimbizi 80,000 waliorundikana kuhamishiwa kwenye sehemu mpya.