Misaada na usawa wa kibiashara vimetajwa kuwa muhimu kusiadia juhudi za kukabiliana na umaskini barani afrika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema kuwa bara la Afrika kwa sasa linahitaji misaada na usawa wa kibiashara na sehemu zingine ili kuliwezesha kukabiliana na umaskini na kupiga hatua zingine za kimaendeleo ili kuweza kufikia malengo ya milenia itimiapo mwaka 2015.
Kupitia ujumbe wake kwenye mkutano wa siku mbili wa nchi za afrika kuhusu malengo ya milenia uliondaliwa mjini Kigali nchini Rwanda, Ban amesema kuwa nchi za Afrika zinahitaji vigezo vitakavyozisaidia kubuni nafasi za ajira na kujisimamia.
Ban amesema kuwa Afrika imepiga hatua katika kupambana na njaa , kupunguza utapia mlo na vifo vya watoto, pia katika sekata ya elimu, kuhakikisha kuwepo kwa maji safi na vita dhidi ya magonjwa ukiwemo ugonjwa wa ukimwi. Akitoa mfano wa Rwanda Ban amesema kuwa kwa sasa asilimia 60 ya watoto nchini humo wanatumia vyandarua vilivyo na dawa vinavyozuia mbu wanaosambaza ugonjwa wa malaria ikiwa ni asilimia kubwa zaidi barani Afrika.