Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban azingatia masuala ya Kulinda amani na kupunguza silaha wakati wa ziara yake Austria

Ban azingatia masuala ya Kulinda amani na kupunguza silaha wakati wa ziara yake Austria

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anakamilisha ziara yake ya wiki moja huko Austria kwa kukutana na rais Heinz Fischer. Akiwa huko alikutana na maafisa wa serikali mjini Vienna na kujadili masuala mbali mbali ikiwa ni pamoja na kazi za kulinda amani na kuangamizwa kwa silaha za hatari duniani.

Katika mazungumzo yake na waziri wa mambo ya nchi za nje Michael Spindelegger walijadili hali huko maeneo ya Balkan na mkutano ujao wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia, MDGS hapa New York baadae mwezi huu.

Akiwa huko Austria hii leo, Bw Ban alitoa taarifa inayolaani vikali mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Lahore na Quetta huko Pakistan. Anasema mashambulio hayo yaliyo walenga kwa makusudi waislamu wa madhehebu ya kishia haiyakubaliki.

Wakati wa ziara yake hiyo alihudhuria pia mkutano wa kila mwaka wa maafisa wa vyeo vya juu wa Umoja wa Mataifa na kujadili jinsi Umoja huo unaweza kukabiliana vizuri zaidi na changamoto zote na namna ya kukidhi vizuri matarajio ya jumuia ya Kimataifa.