Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wajumbe kutoka Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa wafanya mkutano na Benki ya Dunia

Wajumbe kutoka Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa wafanya mkutano na Benki ya Dunia

Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa katika jimbo la Darfur UNAMID ametoa wito kwa Benki ya Dunia kutoa udhamini kwa shughuli hiyo ya kulinda amani kama moja ya njia ya kuhakikisha kuwa amani imerejea katika eneo hilo lililokumbwa na mzozo wa muda mrefu.

Kwenye majadilino yaliyofanyika mjini Khartoum nchini Sudan mkuu wa kikosi cha UNAMID Ibrahim Gambari na makamu wa rais wa Benki ya Dunia barani Afrika Obiageli Ezekwesili walikubaliana kuwa pande hizo mbili zitaendelea kutafuta njia za kurejesha maendeleo katika jimbo la Darfur.

Gambari amesema kuwa huku UNAMID ikiendelea na harakati zake za kutoa usalama na kuwapelekea misaada wale wanayoihitaji, pia itafanya mikakati ya kuusadia umoja wa mataifa na washirika wake kutimiza wajibu wao katika jimbo la Darfur. Kwa upande wake Ezekwesili amesema kuwa jukumu la benki ya dunia litakuwa la kuimarisha hali ya maisha kwa wenyeji wa Darfur hasa kupunguza umaskini akisema kuwa msaada wa dola bilioni nne utapelekekwa katika jimbo hilo.