Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNAIDS aihimiza Dunia kuongeza fedha kupambana na HIV/UKIMWI

Mkuu wa UNAIDS aihimiza Dunia kuongeza fedha kupambana na HIV/UKIMWI

Mkurugenzi mkuu wa mpango wa kupambana na HIV /UKIMWI wa Umoja wa Mataifa Michel Sidibe, amerudia kueleza tena haja ya Jumuia ya Kimataifa kutoa dola bilioni 10 zaidi kusaidia mataifa yanayohitaji ili kufikia malengo yao ya kuhakikisha kwamba mipango ya kuzuia, kutibu na kuhudumia wagonjwa wa Ukimwi inamfikia kila mtu duniani.

Akizungumza baada ya kukamilisha zaira yake ya kwanza Australia Bw. Sidibe alisema, kuna watu milioni 10 hivi sasa wanaoishi na virusi vya HIV wanaosubiri kupatiwa matibabu ya kuokoa maisha yao. Na ikiwa hazitapatikana fedha za kutosha anasema mamilioni ya watu watanyimwa huduma iliyoahidiwa kila mtu.

Ikiwa imebaki wiki chache kabla ya mkutano wa wafadhili kugharimia na kuongeza fedha katika Global Fund, Fuko la Kimataifa kwa ajili ya kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, Bw Sidibe alijadili juu ya kupata na kuimarisha uwekezaji katika mipango ya Ukimwi na mkuu wa idara ya misaada ya Australia Bw peter Baxter. Alimshukuru Bw Baxter kwa msaada wa idara yake kwa mipango hasa ya mataifa ya Asia na Pasific na ahadi yao ya hivi karibuni ya kuongeza mchango wao kwa UNAIDS kwa karibu dola 900 000.