Wakuu wa UNICEF/WFP wato wito wa msaada mpya kwa waathiriwa wa mafuriko Pakistan

31 Agosti 2010

Wakurugenzi wakuu wa Idara ya kuwahudumia watoto UNICEF na Mpango wa Chakula Duniani WFP wametoa wito kwa jumuia ya mataifa hii leo kuongeza msaada wao kwa waathiriwa wa mafuriko yanayoendelea huko Pakistan.

Anthony Lake wa UNICEF na Josette Sheeran wa WFP walitoa wito huo baada ya kutembelea pamoja kazi zinazofanyika huko Muzzafargarh, wilayani Punjab, moja wapo ya maeno yaliyoathirika vibaya sana nchini humo.

Wakati UNICEF na WFP zinazingatia kuokoa maisha ya watu wanaoendelea kukimbia maji ya mafuriko, idara hizo mbili tayari zimeanza miradi ya kukarabati visima na miundo mbinu mingine muhimu. pamoja na kuwasaidia wakulima katika juhudi za kwanza za kurudi katika mashamba yao.

Wakati huo huo idara ya huduma za dharura OCHA, inaeleza kwamba hali huko kusini ya Sindh inabaki kua mbaya na kuna haja ya kuongeza kwa haraka msaada wa Dharura.

Msemaji wa OCHA huko Geneva Elisabeth Byrs anasema vituo vitano vya kuratibu huduma za dharura na kukabiliana na hali huko Sindh vimefunguliwa.

"Idadi ya watu wanaoripotiwa wameathirika moja kwa moja na mafuriko imongezeka na kufikia milioni 17.6. Ingawa maji ya mafuriko yameanza kupungua katika maeneo mengi lakini kuna sehemu za Sindh zinazoendelea kupambana na mafuriko makubwa."

Kwa upande wake shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kwamba nusu milioni ya wanawake waloathirika na mafuriko wanatarajia kuzaa katika kipindi cha miezi sita ijayo huko Pakistan.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter