Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yasema zaidi ya watoto nusu milioni huenda wakazaliwa kwenye dimbwi la mafuriko yaliyoikumba Pakistan

WHO yasema zaidi ya watoto nusu milioni huenda wakazaliwa kwenye dimbwi la mafuriko yaliyoikumba Pakistan

Shirika la afya Ulimwenguni WHO linakadiria kwamba zaidi nusu ya milioni ya kina mama wajawazito ambao wamekumbwa na mafuriko nchini Pakistan watajifungua katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.

Kwa maana hiyo WHO imesema kuwa lazima jitihada ziongezwe ili kuwanusuru kina mama hao pamoja na watoto wao watakaozaliwa ili wasitumbukie kwenye majanga yanayohusiana ya matatizo ya kiafya.

Kulingana na mratibu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na misaada ya usamaria wema, Martin Mogwanja mafuriko hayo tayari yamewaathiri watu milioni 18, hivyo kama jitihada hazitafanyika sasa ulimwengu unaweza kushuhudia watoto zaidi ya nusu milioni wanaotazamiwa kuzaliwa nao wakiangukia mikononi mwa janga hilo.

Tayari mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa ikiwemo, shirika linalohusika na idadi ya watu duniani (UNFPA), (UNICEF) na WHO,zimeanza kutupia jicho namna ya kushughulikia athari za kiafya zinazotokana na mafuriko hayo.