Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la usalama laihimiza DRC kuchunguza ubakaji ulotokea mashariki ya nchi

Baraza la usalama laihimiza DRC kuchunguza ubakaji ulotokea mashariki ya nchi

Wajumbe wa Baraza la usalama wameeleza hasira zao kutokana na mashambulio ya ubakaji wa raia yaliyofanywa na makundi ya waasi huko mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baraza hilo lilitoa pia wito kwa serikali ya Kinshasa kuchunguza kwa haraka shambulio hilo la ubakaji wa karibu watu 154 na kuitaka serikali kuhakikisha kwamba walotenda uhalifu huo wafikishwe mahakamani.

Akisoma taarifa iliyotolewa Alhamisi balozi wa Rashia ambae ni rais wa Baraza la Usalama kwa mwezi huu Vitaly Churkin alisema wajumbe wamerudia ombi lao la kutaka pande zote zinazohusika katika ghasia kusitisha mara moja utumiaji wa ghasia za ngono na ukiukaji wa aina yeyote ya haki za binadam dhidi ya raia.

Wajumbe wa baraza la usalama walipongeza uwamuzi wa katibu mkuu kumpeleka mara moja naibu katibu mkuu Atul Khare kuchunguza mashambulio hayo.

Balozi wa marekani kwenye Umoja wa Mataifa Bi Susan Rice alilaani vikali ubakaji huo. Alisema maelezo yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa juu ya mashambulio ni ya kukera kwa sababu ya yale waloarifiwa na kile ambacho kinahitaji kuchunguzwa. Alisema alipotembelea mashariki ya drc mwaka jana aliambiwa kwamba walinda amani wana taratibu za kutoa onyo la mapema na kujibu kwa haraka.

"Hii leo tumefahamu kamba mara nyingi taratibu hizo hufanya kazi. Lakini safari hii ni wazi hazikufanya kazi na tunahitaji kujua kwa nini na ni utaratibu gani unahitajika kuhakikisha ukatili kama huu hautokei tena na tena."

Baraza limemsifu pia Katibu mkuu kwa kumteua mwakilishi maalum wa ghasia za ngono katika maeneo ya vita Margot Wallstrom kuratibu juhudi za UM katika tukio hilo.