Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO inatathmini upya shughuli zake DRC kufuatia ubakaji wa watu wengi

MONUSCO inatathmini upya shughuli zake DRC kufuatia ubakaji wa watu wengi

Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, MONUSCO Roger Meece amesema ofisi yake inatafakari upta juu ya shughuli zake huko mashariki ya Kongo kufuatia ubakaji wa watu wengi ulofanywa na makundi ya waasi.

Bw Meece aliwambia waandishi habari akiwa mjini Goma kwamba MONUSCO imechukua hatua mpya za kuwalinda raia ikiwa ni pamoja na uongeza kazi za kupiga doria.

Meece alisisitiza kwamba kumekuwepo na juhudi za kuanzisha mawasiliano ya kawaida kati ya raia na maafisa wake wa kiraia huko Goma na maeneo mengine ya Kivu ya Kaskazini.

Afisa huyo alisema kambi yao huko Kibua, iliyoko kilomita 30 kutoka eneo la shambulio la ubakaji imeshachukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya kila wiki na maafisa wa wilaya hiyo ili kuzungumzia matatizo yao. Zaidi ya hayo wanavijiji wataweza kuwasiliana moja kwa moja na maafisa wa kambi ya Kibu kila siku.