Baraza la Usalama linalaani vikali shambulizi dhidi ya hoteli Mogadishu

Baraza la Usalama linalaani vikali shambulizi dhidi ya hoteli Mogadishu

Hali ya ukosefu wa usalama na wasi wasi unaendelea kuwakumba wakazi wa Mogadishu wakati waasi wa Kislamu wakiendela na mashamblizi yao dhidi ya serikali.

Siku ya Jumanne waasi wa kundi la al-Shabab wakivaa mavazi ya jeshi la serikali walishambulia hoteli ya Muna mjini Mogadishu na kusababisha vifo vya raia 30 na wabunge sita. Baadhi ya ripoti zinaeleza kwamba idadi ya vifo mnamo wiki hii pekee huwenda ikawa zaidi ya 80.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu huko Somalia, Augustine Mahiga walilaani vikali shambulio hilo. Wajumbe 15 wa Baraza la usalama walitoa wito wa kukamatwa na kufikisha haraka mahakamani wahusika wa shambulio hilo.

Baraza pia lilisisitiza haja ya kuendelea kuimarisha vyombo vya usalama vya Somalia na umuhimu wa majadiliano yatakayohusisha wadau wote katika utaratibu wa amani.