Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama limejadili utaratibu wa kisheria kukabiliana na uharamia nje ya pwani ya Somalia

Baraza la Usalama limejadili utaratibu wa kisheria kukabiliana na uharamia nje ya pwani ya Somalia

Katibu Mkuu Ban Ki-moon alisisitiza juu ya haja ya kuwepo na mfumo wa kisheria kupambana vilivyo dhidi ya uharamia katika bahari za kimataifa.

Akizungumza kwenye Baraza la Usalama wakati wa mjadala juu ya matatizo ya uharamia nje ya pwani ya Somalia, alisema kwamba mnamo miezi saba iliyopita kumekuwepo na matukio 139 yaliyohusiana na uharamia nje ya pwani ya Somalia.

Katibu Mkuu alieleza kwamba mnamo miaka mitatu iliyopita jumuia ya kimataifa imefanya juhudi kubwa kukabiliana na tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kubuniwa kwa kundi la mawasiliano na kupeleka idadi kubwa ya manwari za kivita katika eneo hilo. Hata hivyo amesema mambo mengi zaidi yanaweza kufanyika hasa kutayarisha mfumo wa kisheria kupambana na janga hilo, akipendekeza hatua saba alizowaslisha kwenye ripoti yake kwa Baraza la usalama.

Baadhi ya hatua hizo amesema ni kuimarisha juhudi zinazoendelea kusaidia mataifa ya eneo hilo kuwahukumu na kuwafunga wanaohusika na vitendo vya uharamia na wizi wa kutumia nguvu baharini.

(SAUTI YA KATIBU MKUU)

Bw Ban Ki-moon alisema hatua ya mwisho ni kwa baraza la usalama kuunda mahakama kamili ya kimataifa chini ya kifungu cha saba cha katiba ya Umoja wa mataifa.