Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idara za UM zinatayarisha mipango kabla ya majira ya baridi huko Kyrgyz

Idara za UM zinatayarisha mipango kabla ya majira ya baridi huko Kyrgyz

Idara za Umoja wa Mataifa zimeanza juhudi za kuhakikisha kwamba maelfu na maelfu ya watu waloathirika na ghasia za hivi karibuni huko Kyrgyzstan wana chakula cha kutosha na makazi ya muda kabla ya kuanza kwa majira ya baridi.

Uchunguzi ulofanywa kote nchini mwezi wa Julai na idara ya Chakula Duniani WFP, umegundua kwamba zaidi ya robo moja ya wakazi wa Kyrgyzstan hawana chakula cha kutosha. Ripoti inaonya kwamba kuna zaidi ya watu 340,000 ambao wako hatarini ya kutokua na chakula cha kutosha mnamo miezi ijayo kutokana na kuzorota kwa hali ya uchumi na majira makali ya baridi wakati akiba ya chakula inapungua.

Idara ya kuwahudumia wakimbizi ya UM inakadiria kwamba kuna watu 750, 000 wangali hawana makazi. Msemaji wa UNHCR Andrej Mahecic anasema UNHCR imeanza kujenga makazi ya muda kwa ajili ya familia zilizopoteza makazi yao.

(SAUTI YA MAHECIC)

Karibu watu laki nne walikimbia makazi yao wakati wa mapigano yalipozuka kati ya makabla ya Kyrgyz na Uzbeks katika wilaya za kusini nchini humo.