Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR inahofia wakimbizi wa Afghanistan walioko Pakistan

UNHCR inahofia wakimbizi wa Afghanistan walioko Pakistan

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linasema linahofia athari za mafuriko kwa wakimbizi wa Afghanistan walioko Pakistan, ambapo baadhi yao wanafikiria kuondoka nchini humo na hasa eneo la Peshawar.

Kwa mijubu wa UNHCR kati ya wakimbizi milioni 1.7 wa Afghanistan , nchi ya Pakistan ndio iliyo na idadi kubwa ya wakimbizi hao, zaidi ya milioni 1.5 wako katika majimbo yaliyoathirika na mafuriko huku vijiji kadhaa vya Waafghanistan vikiwa vimeharibiwa vibaya na mafuriko na vingine kusambaratishwa kabisa.

Mengi ya makazi ya wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistan yalianzishwa miaka 30 iliyopita baada ya uvamizi wa muungano wa Soviet kusababisha wimbi la kwanza la wakimbizi.

Wakati huohuo UNHCR imekaribisha hakikisho la serikali ya Pakistan kwamba watu wote walioathirika na mafuriko wataweza kurejea majumbani kwao kujijenga upya wakiwemo wakimbizi wa Afghanistan ambapo kamishna wa wakimbizi nchini Afghanistan amesema wakimbizi pia wanahaki ya kurejea kwenye makambi yao.