Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wenye ulemavu wanaweza kuchangia pakubwa kwenye uchumi wa Asia-Pasicific:UM

Watu wenye ulemavu wanaweza kuchangia pakubwa kwenye uchumi wa Asia-Pasicific:UM

Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliomalizika leo mjini Bangkok Thailand umezichagiza biashara kuzingatia haki na mahitaji ya wenye ulemavu, ukisema kwamba wanamchango mkubwa katika biashara kama wateja.

Katika mkutano huo wa siku mbili wa ushirikiano wa kanda ya Asia kuhusu watu wenye ulemavu washiriki zaidi ya 60 wamehudhuria ikiwa ni pamoja na maafisa wa serikali, wawakilishi wa biashara, watu wenye ulemavu na mashirika mbalimbali.

Mkutano huo umejadili njia ambazo mipango ya maendeleo na ajira itakavyoweza kuwajumuisha pia wenye ulemavu. Inakadiriwa kuwa watu milioni 400 wenye ulemavu wako katika kanda ya Asia-Pacific.

Mkutano huo uliofanyika kwenye tume ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na jamii kwa asia na Pacific ESCAP mjini Bangkok umetoa azimio linalowataka viongozi kuweka mipango ya maendeleo ya biashara kama kipaumbele kwa wenye ulemavu katika muongo ujao kuanzia mwaka 2013.