Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa UM alaani shambulio dhidi ya MUNUSCO DRC

Katibu Mkuu wa UM alaani shambulio dhidi ya MUNUSCO DRC

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani mauaji ya walinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika taarifa iliyotolewa leo Ban amesema ameshtushwa na vifo hivyo wa walinda amani kutoka India waliokuwa wakihudumu na mpango wa Umoja wa Mataifa Congo MUNUSCO. Walinda amani hao watatu waliuawa alfajiri ya leo baada ya shambulio la kushtukiza na watu waliokuwa na silaha kwenye kituo chao cha Kirumba Mashariki mwa Congo kwenye jimbo la kivu.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky walinda amani wengine sita wamejeruhiwa katika shambulio hilo na watatu kati yao vibaya sana. Nesirky amesema Katibu Mkuu ametoa salamu za rambirambi kwa serikali ya India na familia za wanajeshi hao waliouawa. Na ameitaka serikali ya Congo kufanya uchunguzi mara moja kuhusu shambulio hilo na kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.