Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfuko wa UM watoa dola milioni 27 kusaidia Pakistan

Mfuko wa UM watoa dola milioni 27 kusaidia Pakistan

Mamilioni ya watu walioathirika na mafuriko nchini Pakistan watapokea msaada wa haraka kufuatia dola milioni 27 zilizotolewa na mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF.

CERF imetoa fedha hizo kuyasaidia mashirika ya misaada ya kibinadamu kuchukua hatua kuwasaidia wanaohitaji msaada wa haraka nchini Pakistan amesema John Holmes mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na msaada wa dharura.

Holmes ameongeza kuwa idadi ya vifo si kubwa sana ikilinganishwa na majanga mengine makubwa, lakini amesema idadi ya walioathirika ni kubwa sana na kama hatua hazitochukuliwa sasa ameonya kuwa vifo vitaongezeka.

Shirika la mpango wa chakula WFP litatumia fedha za CERF kutoa msaada wa haraka wa chakula kwa watu takribani milioni 4 katika maeneo yaliyoathirika zaidi na mafuriko. Nayo mashirika ya UNHCR, IOM, WHO, UN-HABITAT na UNICEF watatumia fedha za CERF kutoa msaada wa malazi, vifaa vya kupikia, madawa, maji safi na huduma za afya.