Wafanyakazi wa UNAMID waliotekwa Darfur waachiliwa
Taarifa kutoka El-fasher Sudan zinasema raia wawili wa Jordan ambao ni washauri wa polisi wa mpango wa kulinda amani Darfur wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID waliotekwa Jumamosi iliyopita leo wameachiliwa huru.
Walinda amani hao waliachiliwa kwenye eneo la Kass Kusini mwa Darfur, na wakasafirishwa mara moja hadi kwenye hospitali ya UNAMID Nyala ambako wanafanyiwa uchunguzi wa afya. Wanaonekana kutodhuriwa na wako kwenye afya nzuri na baadaye wanatarajiwa kupelekwa mjini Khartoum.
Kuachiliwa kwao kumefuatia mkutano wa jana Nyala kati ya Bwana Yonis ambaye ni afisa msaidizi wa vikosi vya UNAMID na kamati ya pamoja ya UNAMID na serikali ya Sudan iliyoundwa kutatua suala hilo.