Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 20 ya fedha za msaada zilizoombwa na UM kwa ajili ya Pakistan wiki hii zimepatikana

Asilimia 20 ya fedha za msaada zilizoombwa na UM kwa ajili ya Pakistan wiki hii zimepatikana

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA linasema asilimi 20 ya msaada wa dola milioni 460 zilizoombwa jumatano wiki hii na Umoja wa Mataifa umepatikana.

OCHA inasema hadi sasa wanazo fedha taslim dola milioni 147 na milioni 87 ni ahadi. Na mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kupeleka msaada wake ili kukidhi mahitaji ya mamilioni ya watu walioathirika na mafuriko. Utabiri wa hali ya hewa nchini Pakistan umetoa tahadhari kwamba mvua zitaendelea kunyesha na huenda mafuriko yakaendelea kusambaa katika majimbo ya Punjab, Sind na Balochistan katika mwezi mmoja ujao.

Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema pamoja na matatizo ya kuweza kuwafikishia msaada waathirika wote, linafurahi kwamba limeweza kuwapa watu 430,000 mgao wa chakula wa mwezi mmoja. Emilia Casella ni msemaji wa WFP

(SAUTI YA EMILIA CASELLA)

Kuhusu masuala ya afya shirika la afya duniani WHO linasema wilaya 56 kati ya 74 zilizoathirika na mafuriko zimeweza kupata taarifa kuhusu magonjwa ya mlipuko. Shirika hilo linasema kuna hofu ya magonjwa kama kuhara na kipindupindu lakini linaamini kwa taarifa wanazotoa kila siku zitasaidia.

Nalo shirika la kuhudumia watoto UNICEF linasema katika siku tatu zilizopita watoto, kina mama wajawazito na wanaonyonyesha wamepewa chanjo dhidi ya surua, polio na pepo punda katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika na mafuriko nchini Pakistan, kama anavyofafanua msemaji wa UNICEF Marco Rodriguez.

(SAUTI YA RODRIGUEZ)