Zaidi ya watoto milioni 2 wanahitaji msaada haraka Pakistan:UNICEF
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF linasema watoto milioni sita wameathirika na mafuriko nchini Pakistan na milioni 2.7 kati yao wanahitaji msaada wa haraka kuokoa maisha yao.
Kwa mujibu wa makadirio ya Umoja wa Mataifa watu milioni 14 wameathirika na mafuriko. Maelfu wameshapokea msaada lakini mamilioni zaidi wanahitaji malazi, chakula, maji na huduma za afya.
Mwakilishi wa UNICEF nchini humo Martin Mogwanja amesema hali inaweza kuwa mbaya zaidi jimbo la Sindh kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema hili ni janga kubwa kabisa kuwahi kuikumba Pakistan na ukanda mzima katika kumbukumbu zake, ambapo mamilioni ya wanawake na watoto wako katika hali mbaya. Ameongeza kuwa haya ni mashindano dhidi ya wakati, kwa sasa wanahitaji kuandaa mazingira ya dharura kwa watu milioni 1.8 wasio na makazi. Miongoni mwa msaada unaotolewa na UNICEF ni madawa,lishe, maji na vifaa vya usafi, ulinzi kwa watoto na elimu.