Mashirika ya UM yametoa wito wa msaada wa dola milioni 460 kusaidia waathirika wa mafuriko Pakistan

11 Agosti 2010

Umoja wa Mataifa na washirika wake wanahitaji dola milioni 459.7 katika wiki chache zijazo ili kukidhi mahitaji ya haraka ya mamilioni ya watu walioathirika na mafuriko nchini Pakistan.

Akizungumza kwenye uzinduzi maalumu wa msaada huo wa kibinadamu kwa ajili ya watu wa Pakistan kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa New York, mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa John holmes amesema wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanaohitaji msaada wanaupata lakini cha msingi zaidi ni kupata fedha.

(SAUTI YA JOHN HOLMES)

Serikali ya Pakistan inakadiria kuwa watu milioni 14 wameathirika na mafuriko hayo, kwa sasa imetoa helkopta zinazoyasaidia mshairika ya msaada kusambaza huduma kama anavyoeleza Emilia Casella msemaji wa shirika la mpango wa chakula WFP

(SAUTI YA EMILIA CASELLA)

Kati ya fedha zilizoombwa dola milioni 105 zinahitajika kuwasaidia watu zaidi ya milioni mbili amesema mratibu wa masuala ya kibinadamu nchini Pakistan Martin Mogwanja. Ameongeza kuwa dola zingine milioni 150.5 zitatumika kwa chakula, huku milioni 5.7 zitahitajika kuhakikisha usalama wa mifugo.

 Watu zaidi ya 1200 wamekufa tangu kuanza kwa mvua za monsoon 22 Julai mwaka huu. Kwa sasa mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na shirika la kimataifa la uhamiaji wanapanga kuwasaidia mamilioni ya waathirika katika maeneo ya Baluchistan, Punjab, Gilgit Baltistan, KPK, Kashmir na Sindh.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter