Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waainisha mipango ya kukabiliana na tishio la usalama Jamhuri ya Afrika ya Kati

UM waainisha mipango ya kukabiliana na tishio la usalama Jamhuri ya Afrika ya Kati

Umoja wa Mataifa umependekeza kuimarisha uwezo wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ili kuiwezesha kukabiliana vilivyo na changamamoto za usalama na za kibinadamu wakati vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vitakapoondoka.

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na Chad MINURCAT ulianzishwa na baraza la usalama mwaka 2007 kusaidia kulinda raia na shughuli za misaada kwa maelfu ya watu waliosambaratishwa na vita katika nchi hizo mbili na nchi jirani ya Sudan. Sasa vikosi hivyo vinatarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwaka.

Baraza lilipiga kura mwezi Mai kumaliza mpango wa MINURCAT ifikapo Desemba 31 baada ya serikali ya Chad kuomba uondoke na kusema kwamba itachukua jukumu la kuwalinda raia wake nchini mwake.

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu na mkuu wa MINURCAT Youssef Mahmoud amesema suluhu ya haraka lazima ipatikane katika miezi miwili ijayo kuzima pengo la usalama kufuatia kuondoka kwa MINURCAT eneo la Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu kwenye baraza la usalama Bwana Mahmoud amesema tishio la usalama kwa raia, wakimbizi wa ndani, wakimbizi wa kawaida na wafanyakazi wa misaada bado ni kubwa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.