Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afisa wa UM aonya juu ya kesi ya akari mtoto anayeshikiliwa Guantanamo

Afisa wa UM aonya juu ya kesi ya akari mtoto anayeshikiliwa Guantanamo

Afisa wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa kesi ya leo kwenye tume ya kijeshi ya Guantanamo Bay dhidi ya Omar Khadr aliyekamatwa Afghanistan 2002 kwa uhalifu anaodaiwa kufanya akiwa mtoto , inaweza kutoa ishara itakayoweka matatani hali ya askari watoto kote duniani.

Bi Radhika Coomaraswamy ambaye ni mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu kwa ajili ya watoto kwenye vita vya kutumia silaha amesema Khadr alikuwa na umri wa miaka 15 tuu wakati aliposhutumiwa kuvurumisha gruneti lililomuua mwanajeshi wa Marekani, na sasa anakabiliwa na makosa ya uhalifu wa vita.

Bi Coomaraswamy amesisitiza kuwa mkataba wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC uko wazi kwamba hakuna yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 anayestahili kufunguliwa kesi ya uhalifu wa kivita. Ameongeza kuwa tangu vita ya pili ya dunia hakuna mtoto aliyehukumiwa kwa uhalifu wa vita, watoto lazima wachukuliwe kama waathirika na hatua mbadala zichukuliwe hasa kuwasaidia kuwarejesha katika maisha ya kawaida.