Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya raia Afghanistan vimeongezeka kwa asilimia 31:UNAMA

Vifo vya raia Afghanistan vimeongezeka kwa asilimia 31:UNAMA

Ripoti ya katikati ya mwaka 2010 ya mpango wa msaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA inasema mbinu za Taliban na makundi mengine yanayopinga serikali AGE\'S vimesababisha ongezeko la vifo vya raia kwa asilimia 31 kutokana na vita.

Takwimu hizo ni za kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu wa 2010. Miongoni mwa waliouawa au kujeruhiwa na Taliban na AGEs ni watoto asilimia 55 zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana 2009, huku idadi ya wanawake ikiongezeka kwa asilimia sita. Vifo vya majeshi yanayounga mkono serikali vimepungua kwa asilimia 30 katika kipindi hicho kwa sababu ya kupungua kwa asilimia 64 ya vifo au majeruhi wa mashambulizi ya anga.

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan Staffan de Mistura amesema kitengo cha haki za binadamu cha UNAMA imesema jumla ya raia 3268 wameathirika katika kipindi hiki, vifo vikiwa 1271 na majeruhi 1997.  Na AGEs wamehusika na mauaji ya watu 2477 ikiwa ni asilimia 76 ya mauaji yote .

Hilo ni ongezeko la asilimia 53 ikilinganishwa na mwaka 2009. Kitengo kimetoa mapendekezo kwamba Taliban na AGEs waondoe amri zote za mauaji ya raia, kutumia raia kama ngao na mashambulizi ya kujitoa muhanga ili waweze kutimiza sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu.