Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umetaja majina ya wajumbe wa Israel na Uturuki katika kamati ya uchunguzi wa flotilla

UM umetaja majina ya wajumbe wa Israel na Uturuki katika kamati ya uchunguzi wa flotilla

Wajumbe wa Israel na Uturuki watakaoshiriki tume ya uchunguzi wa tukio la meli ya misaada ya flotilla iliyokuwa ikielekea Gaza Mai 31, wametajwa.

Katika taarifa yake iliyotolewa mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemtaja mjumbe wa Israel kuwa ni Bwana Joseph Ciechanover na wa Uturuki kuwa ni Bwana Ozdem Sanberk. Amesema watu hao wawili wana rekodi nzuri katika masuala ya huduma za jamii na anatarajia kukutana nao kesho Jumanne Agosti 10 mjini New York ambako watakutana na wajumbe wengine wa tume.

Wajumbe wengine wa tume hiyo ni waziri mkuu wa zamani wa New Zealand bwana Geoffrey Palmer ambaye ndio mwenyekiti wa tume, na Rais wa zamani wa Colombia Bwana Alvaro Uribe ambaye ni makamu mwenyekiti.

Watu tisa waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa wakati jeshi la Israel liliposhambulia meli sita ambazo zilikuwa zikisafiri kutoka Uturuki kuelekea Gaza zikijaribu kukiuka vizuizi vya usafiri vilivyowekwa na Israel kuingia Gaza.