Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon ametangaza jopo la kushughulikia masuala ya kimataifa

Ban Ki-moon ametangaza jopo la kushughulikia masuala ya kimataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon leo ametangaza jopo maalumu la watu watakaoshughulikia masuala ya kimataifa.

Jopo hilo litaongozwa na uwenyekiti wa Rais Tarja Halonen wa Finland na Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini. Wajumbe wengine wa jopo hilo ni pamoja na watu mashuhuri duniani, waunda sera kutoka katika serikali, wafanyabiashara na jumuiya za kijamii. Kazi kubwa ya jopo hilo itakuwa ni kushugulikia jinsi ya kutokomeza na kuwaondoa watu katika umasikini, huku wakiheshimu na kulinda hali ya hewa na mifumo ya asili inayotusaidia kuishi.

Ban amesema ameliambia jopo hilo kuwa na mtazamo mpana kwani mawazo na ajenda finyu zimeshapitwa na wakati. Ameongeza kuwa dunia inahitaji kupunguza gesi ya cabon ili kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa. Jopo hilo linatarajiwa kutoa ripoti mwishoni mwa mwaka 2011 wakati ambao pia kutakuwa na maandalizi ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo endelevu utakaofanyika mjini Rio de Janeiro mwaka 2012.