Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya walioathirika na mafuriko Pakistan imepindukia milioni 6:UM

Idadi ya walioathirika na mafuriko Pakistan imepindukia milioni 6:UM

Idadi ya walioathirika na mafuriko nchini Paskistan imearifiwa kuzidi milioni 6, na kuongeza hofu juu ya hatma ya maelfu ya watu waliokwama kutokana na mafuriko hayo bila msaada.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa makadirio ya majimbo yaliyoathirika zaidi ya Baluchistan, Punjab na Khyber Pakhtunkhwa KPK kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa. Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini humo Martin Mogwanja amesema hali itakuwa mbaya zaidi kabla ya kuanza kutengamaa, na ameongeza kuwa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanafanya kila juhudui kuwafikia waathirika.

Mafuriko hayo sasa yamefika jimbo la Sindh kusini mwa Pakistan ambako mamia ya vijiji vimefurika na mtaalamu wa majanga wa Umoja wa Mataifa Dennis Bruhn amesema hakuna takwimu halisi lakini maelfu au mamilioni ya watu wameathirika katika jimbo hilo. Kwa mujibu wa utabiri wa hali ya hewa mvua zinaendelea kunyesha katika jimbo hilo kwa siku tatu zijazo.