Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM umetoa wito wa juhudi zaidi za kuzisaidia jamii za watu wa asili duniani

UM umetoa wito wa juhudi zaidi za kuzisaidia jamii za watu wa asili duniani

Leo ni siku ya kimataifa ya watu wa asili duniani, katika ujumbe maalumu wa kuadhimisha siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema watu wa asili ndio wanaongea lugha nyingi kwa asilimia kubwa, wamerithi na kuendeleaza utajiri wa elimu, mifumo ya sanaa, dini na utamaduni, na hivyo tunarejea wito wa kujali maslahi yao.

Ban amesema watu wa asili bado wanabaguliwa, ndio walio na matatizo ya afya na wana umasikini mkubwa, na katika sehemu mbalimbali lugha zao, utamaduni wao na dini zao zinanyanyapaliwa na kudharauliwa, hivyo dunia inahitaji kuchukua hatua zaidi kuwalinda watu hawa.

Naye mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu na uhuru wa watu wa asili James Anaya amesema watu wa asili ambao ni fukara miongoni mwa masikini haki zao za binadamu zinaendelea kukiukwa. Miongoni mwa watu hao wa asili Afrika ni Waturkana kutoka nchini Kenya.

(RIPOTI JASON NYAKUNDI)