Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlimbwende Naomi Campbell atoa ushahidi ICC dhidi ya Charles Taylor

Mlimbwende Naomi Campbell atoa ushahidi ICC dhidi ya Charles Taylor

Mlimbwende wa kimataifa Naomi Campbell amesema alipewa mawe machafu baada ya chakula cha usiku kilichohudhuriwa pia na aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor.

Mwanamitindo huyo alikuwa akitoa ushahidi kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC mjini The Hauge dhidi ya kesi ya Taylor kuhusu madai kwamba alimpa Naomi almasi mwaka 1997. Waendesha mashitaka katika mahakama hiyo wamesema ushahidi wake unaweza kusaidia kumuhusisha bwana Taylor na mawe hayo, ambayo anashutumiwa kuyatumia kufadhili vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone.

Katika ushahidi wake bi Campbell amesema alipewa mawe mawili au matatu baada ya chakula cha jioni nchini Afrika ya Kusini, kilichoandaliwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo Nelson Mandela.

Ameongeza kuwa kabla ya kukutana na bwana Taylor alikuwa hajawahi kumsikia, wala kuisikia nchi ya Liberia. Amesema alipewa mawe hayo na kuyafungua siku iliyofuata na kwa wakati huo hakujua sheria zozote kuhusu almasi ambazo hazijachongwa.