Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan yatakiwa kuongeza juhudi ikijiandaa kwa kura ya maoni:UM

Sudan yatakiwa kuongeza juhudi ikijiandaa kwa kura ya maoni:UM

Afisa wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa haja ya kuongeza juhudi za kutatua masuala muhimu yakiwemo ya uraia na mipaka kabla ya kura ya maoni nchini Sudan.

Alain LeRoy ambaye ni mkuu wa masuala ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa amesema ingawa anakaribisha hatua ya pande mbili nchini Sudan za mkataba wa amani kumaliza vita baina ya Kaskazini na

Kusini na kukubali kuitisha kura ya maoni, lakini pande hizo mbili lazima zishughulikie masuala hayo. Sudan itapiga kura mapema mwakani kuamua endapo igawike mapande mawaili yaani Kusini ijitenge na pia kuamua hatma ya Abyei eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta katikati mwa nchi hiyo.

Kura hiyo ya maoni ni sehemu ya makubaliano ya amani ya mwaka 2005 CPA ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda mrefu. Kwa upande wake mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan UNMIS unajiandaa kwa kura hiyo ya maoni kwa kusaidia msaada wa kiufundi.