WHO imepeleka msaada wa madawa kwa waathirika wa mafuriko Afghanistan

WHO imepeleka msaada wa madawa kwa waathirika wa mafuriko Afghanistan

Shirika la afya duniani WHO leo limeanza kupeleka msaada wa haraka wa madawa kwa maelfu ya watu walioathirika na mafuriko nchini Afghanistan.

Mwakilishi wa WHO nchini humo Peter Graaf amesema hofu kubwa hivi sasa ni maji ambayo yatasababisha kusambaa kwa magonjwa ya kuambukiza. Ameongeza kuwa WHO inaisaidia serikali ya Afghanistan kukabiliana na mahitaji ya afya katika majimbo yaliyoathirika na mafuriko hayo, ili kuhakikisha mahitaji ya haraka ya afya yanafikiwa.

Serikali inasema mafuriko hayo yamewaacha maelfu bila makazi katika maeneo ya Kapisa, Katikati mwa Ghazni, Nangarhar, Kunar, Logar, Khost na kaskazini mwa Parwan. Hadi sasa WHO kwa ombi la serikali ya Afghanistan imeshatoa msaada wa madawa na vifaa vya matibabu vya kuweza kusaidia watu 9000 na kutibu wagonjwa wa kuhara 5000.