Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo endelevu ni kiini cha kufikia malengo ya milenia wasema UM

Maendeleo endelevu ni kiini cha kufikia malengo ya milenia wasema UM

Maendeleo endelevu yameelezwa kutoa mikakati na mtazamo utakaosaidia kuratibu na kuchukua hatua za kufikia malengo ya maendeleo ya milenia.

Mtazamo huo umetolewa na afisa wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya uchumi na jamii Sha Zukang. Bwana Zukang ameuambia mkutano wa mawaziri wa tathimini ya malengo ya maendeleo ya mileni kwa nchi za Asia-Pacific uliomalizika leo mjini Jakarta Indonesia kwamba , maendeleo endelevu pekee yakiwa na vigingi vitatu ambayo ni maendeleo ya kijamii, ukuaji wa uchumi na kulinda mazingira ndiyo yanatakayoshughulikia mahitaji ya sera kwa ajili ya kufikia malengo ya milenia.

Katika ujumbe maalumu aloutoa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon kwenye mkutano huo amesema eneo la Asia-Pacific limepiga hatua kubwa katika kuchangia kwenye mafanikio ya dunia. Ban amesema mkutano huo ni muhimu kubaini mikakati gani iliyofanikiwa katika nchi zao na kuangalia ni jinsi gani mafanikio yao yanaweza kuwa chachu sehemu zingine.

Ameongeza kuwa baadhi ya nchi zimekuwa na mafanikio katika kukabiliana na njaa, kuongeza idadi ya watoto wanaoandikishwa shule, afya ya mtoto, uwezo wa kupata maji safi na matibabu ya HIV na kudhibiti kifua kikuu, malaria na magonjwa mengine. Amesema mafanikio hayo yametokea katika baadhi ya nchi masikini kabisa na kudhihirisha kwamba malengo ya maendeleo ya milenia yanaweza kufikiwa. Ingawa amesema mafanikio hayo yanatofautiana katika kila lengo na katika kila nchi.