Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marufuku kumpiga picha Naomi Campbell wakati wa ushahidi dhidi ya Charles Taylor

Marufuku kumpiga picha Naomi Campbell wakati wa ushahidi dhidi ya Charles Taylor

Majaji katika mahakama ya kimataifa ya the Hague wamekataza mwanamitindo maarufu Naomi Campbell kupigwa picha anapotoa ushahidi katika kesi ya aliyekuwa Rais wa Liberia Charles Taylor.

Bi Campbell, mwenye umri wa miaka 40, anatarajiwa kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo ya uhalifu wa kivita  kesho Alhamis. Bi Campbell ataulizwa juu ya madai kuwa Bw Taylor alimpa almasi haramu zinazotumika kugharamia vita ambazo hazijachongwa kutoka Sierra Leone, baada ya hafla ya chakula cha jioni cha watu mashuhuri iliyofanyika mwaka 1997. Pia ataruhusiwa kupata msaada wa ziada kutoka kwa wakili wake wakati anapotoa ushahidi wake.

Wapiga picha watazuiwa kupiga picha wakati anapoingia na kutoka ndani ya mahakama hiyo.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo ilisema shauku kubwa ya vyombo vya habari katika kesi hiyo imesababisha kuwepo kwa sababu za wasiwasi wa usalama wa Bi Campbell. Bw Taylor anatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika kipindi cha miaka 10 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Sierra Leone. Amekana mashtaka na amesema hajawahi kuhusika na lolote kuhusiana na almasi.

Lakini upande wa mashtaka ulisema wakati vita vikiendelea Sierra Leone, Bi Campbell na Bw Taylor wote walikuwa wageni waalikwa katika shughuli iliyoandaliwa na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela. Baada ya chakula hicho cha jioni, inadaiwa kwamba, wafuasi wawili wa Bw Taylor walikwenda kwenye chumba cha Bi Campbell na kumpa almasi kubwa ambayo haikukatwa.