Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu ya vijana kufaidika na mafunzo ya mradi mpya wa UM Ivory Coast

Maelfu ya vijana kufaidika na mafunzo ya mradi mpya wa UM Ivory Coast

Vijana 3000 nchini Ivory coast, wakiwemo wapiganaji wa zamani na wanawake watapata mafunzo ya ujenzi, kazi za viwandani na sekta za huduma chini ya mradi mpya wa Umoja wa Mataifa .

Mradi huo una lengo la kuwasaidia watu hao kujihusisha na uinuaji wa uchumi wa taifa. Mradi huo wa miaka miliwi utakaogharibu dola milioni 3.5, umeandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya viwanda UNIDO na utajihusisha na mipango ya kuwarejesha watu hao katika maisha ya kawaida, baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 2000 vilivyoigawa mapande nchi hiyo.

Katika mradi huo ambao unafadhiliwa na serikali ya Japan na kutekelezwa mjini Bouake , UNIDO itajenga kituo ambacho kitakuwa kinatoa mafunzo mbalimbali kama uchomeleaji vyuma, ufundi makenika, useremala, ufundi bomba, ujenzi, ushonaji, huduma za afya na masuala ya lishe.