Machafuko yanayoendelea Beni DR Congo yawagungisha virago maelfu

30 Julai 2010

Watu wapatao 90,000 wamearifiwa kuzikimbia nyumba zao eneo la Ben jimbo la Kivu ya Kaskazini nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia operesheni za kijeshi baina ya serikali, wapiganaji wa kundi la FARDC na pia muungano wa jeshi la ukombozi Uganda ADF-NALU.

Tangu kuanza kwa operesheni hizo mauaji mapya yamekuwa yakiarifiwa na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu. Vijiji vimeporwa, watu kushambuliwa, na wengine kulazimika kukimbia hasa wanawake na watoto wakihofia usalama wao. Wiki hii watu sita wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika miji ya Eringeti na Mutwanga Kusini mwashariki mwa Beni.

Mashirika ya misaada katika maeneo hayo yanasema wakimbizi wakimiminika kwenye vituo vya misaada na pia kutafuta hifadhi mashuleni, makanisani na wengine kuhifadhiwa na watu. Duru zinasema watu hao wanahitaji msaada wa haraka wa ulinzi, chakula, maji, malazi, madawa na vitu vingine visivyo chakula. Hivi sasa Umoja wa Mataifa, mashirika yasiyo ya kiserikali na kamati ya kimataifa ya chama cha msalaba mwekundu ICRC ndio wanaotoa msaada kwa watu hao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud