Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani kambi ya Kalma Sudan wataka ulinzi wa UNAMID

Wakimbizi wa ndani kambi ya Kalma Sudan wataka ulinzi wa UNAMID

Maelfu ya wakimbizi wa ndani katika kambi ya Kalma kusini mwa Sudan wamekusanyika nje ya kituo cha ulinzi cha mpango wa kulinda amani Darfur wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika UNAMID, kufuatia ghasia za jana zilizosababisha vifo kadhaa.

Mvutano huo umesababishwa na baadhi ya wakimbizi hao kushiriki mazungumzo ya amani Doha, na ulishika kasi jana mchana baada ya mamia ya wakimbizi kuandamana katika mitaa ya kambi hiyo wengine wakipinga mazungumzo ya amani, huku wengine wakiyaunga mkono. Wengi walikuwa na silaha kama fimbo na mapanga, na milio ya risasi ilisikika kambini Kalma. Zaidi ya watu 7000 wengi wakiwa wanawake na watoto wamekimbilia kuomba ulinzi kwa kituo cha UNAMID ambako wanaamini kuna usalama.

Naibu mwakilishi wa UNAMID Mohamed Yonis amezitaka pande zote kujaribu kuzuia machafuko zaidi kwani ghasia zitaongeza adha kwa wakimbizi hao. Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amezitolea wito pande zote kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani na mazungumzo na kuepuka machafuko.