Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP inaona mapinduzi katika kupambana na baa la njaa barani Afrika

WFP inaona mapinduzi katika kupambana na baa la njaa barani Afrika

Watu wengi katika nchi za Afrika wanaweza kurejea katika hali ya kawaida haraka kutoka kwenye vita na maisha yao kubadilika kupitia mapinduzi ya kupambana na njaa, ikiwemo fursa za kutawala nguvu ya masoko.

Hayo yamesema na mkurugenzi wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP Josette Sheeran mjini Kigali Rwanda leo wakati wa siku ya mwishoo ya ziara yake ya siku nne . Bi sheeran amesema ametiwa moyo kutokana na ari na kujidhatiti kufanya mabadiliko aliyoisikia kwa kila mtu, kuanzia viongozi wa Umoja wa Afrika hadi waathirika wa vita na umasikini.

Amesema nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda na Rwanda, watu wanaganga yajayo kuliko kusalia kwa yaliyopita ya umwagaji damu na vita. Amesema amebaini kwamba masikini, wakimbizi wa ndani na wakulima wadogowadogo wana hamasa ya kutumia njia mpya ili kudhibiti maisha yao, kwa sababu hakuna anayetaka kuwa tegemezi.

Amesema WFP ina mpango wa kununua chakula kutoka nchi 16 za Afrika na Uganda ni miongoni mwao. WFP inawawezesha Waganda kuuza ziada ya mazao yao kwa bei muafaka ili chakula hicho kitumike kuwalisha watoto wenye njaa sehemu nyingine za Afrika. Bi Sheeran amesisitiza kwamba kwa ujumla hali hii yote inawapa uwezo watu kuweza kulikabili tatizo la njaa huku wakisaidia kuitokomeza njaa Afrika.