Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM waikabidhi Liberia jela mpya kama msaada wa ujenzi mpya wa nchi hiyo

UM waikabidhi Liberia jela mpya kama msaada wa ujenzi mpya wa nchi hiyo

Naibu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia ameihakikishia nchi hiyo kuendelea kupata msaada wa Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na kujengwa gereza jipya lililofadhiliwa na Umoja wa Mataifa na pia kituo ambacho wanajeshi wa kulinda amani watakitumia kuitoa mafunzo kwa vijana.

Henrietta Mensa-Bonsu ambaye ni naibu mwakilishi maalumu wa utawala wa sheria kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMIL, amekabidhi gereza la Sanniguellie lililoko mkoani Nimba kwa Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia. Gereza hilo limejengwa kwa ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na wizara ya sheria ya nchi hiyo kwa gharama ya dola 350,000, zilizotolewa na mfuko wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya amani, ambao unazisaidia nchi zilizotoka kwenye vita.

Gereza hilo lina uwezo wa kuhifadhi wafungwa 72, kukiwa na maeneo ya wanaume na wanawake,umeme, vyoo, jiko , mahali pa kupumzikia, pampu ya maji inayotumia umeme wa jua na pia ina uwezo wa kuvuna maji ya mvua ili kuhakikisha huduma ya maji haikatiki.