Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu zaidi ya 100 wahofiwa kufa maji DR Congo baada ya boti kuzama

Watu zaidi ya 100 wahofiwa kufa maji DR Congo baada ya boti kuzama

Watu zaidi ya 100 wahofiwa kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama kwenye mto Congo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa kiongozi wa eneo la Maluku kulikotokea ajali hiyo amesema boti ilizama Jumatatu usiku wakati ikisafiri kutoka Bandudu kuelekea Vanga, maiti 49 zimepatikana na kuzikwa na juhudi zinaendelea kutafuta miili mingine au walionusurika kwa msaada wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo MUNUSCO.

Waziri wa habari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Lambert Mende Omalanga amesema idadi ya waliothibitika kufa hadi sasa ni 80. Maluku ndio mpaka kati ya mji mkuu Kinshasa na mkoa wa Bandudu, na duru zinasema boti hiyo ilikuwa na watu zaidi ya 200. Hali mbaya ya hewa, watu na mizigo kupita kiasi vimeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo. Baadhi ya walionusurika walipelekwa hospitali ya Maluku kilometa 80 nje ya mji wa Kinshasa.