Baraza kuu la UM limetangaza kwamba kupata maji safi na salama ni haki ya binadamu

28 Julai 2010

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa leo limetangaza kwamba maji na usafi ni haki ya binadamu kwa wote.

Limesema maji safi na salama ya kunywa ni muhimu kwa ajili ya maisha ya binadamu na mazingira yake.

Baraza limezitaka nchi zote na mashirika yote ya kimataifa kutoa msaada wa fedha, uwezo na teknolojia kwa kupitia misaada ya kimataifa na ushirikiano hususan kwenye nchi zinazoendelea ili kuchagiza juhudi za kuhakikisha maji safi na salama yanapatikana na kwa gharama nafuu kwa wote. Na pia limekaribisha uamuzi wa baraza la haki za binadamu wa kuomba wataalamu binafsi wa masuala ya wajibu wa haki za binadamu na maji, kuwasilisha ripoti kwenye barala kuu la Umoja wa Mataifa.

Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP mwaka 2003 ilizindua mradi iliouita maji ya kunywa na usafi kwa ajili ya milenia. Mradi huo umesaidia sehemu mbalimbali za Afrika, umetoa fursa kubwa kwa wanawake na watoto. Na una nia ya kuhakikisha watu milioni 2.3 walioko vijijini Senegal wanapata huduma ya maji na kuwafikia asilimia 82 ya watu wanaopata huduma hiyo ifikapo mwaka 2015 ambao ndio mwisho kufanikisha malengo ya maendeleo ya milenia.

(SAUTI YA REGINA DUNLOP)

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter