Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa AU wajitoa kimasomaso kusaidia kuleta amani Somalia

Viongozi wa AU wajitoa kimasomaso kusaidia kuleta amani Somalia

Viongozi hao katika mkutano wao wa 15 uliomalizika leo mjini Kampaka Uganda, wamesema hali ya usalama Somalia bado iko njia panda.

Wamesema jambo hilo linaziweka pia nchi jirani katika hofu, ukizingatia ni hivi majuzi tuu wanamgambo wa Al-Shabab kutoka nchini humo wamekiri kuhusika na mashambulio ya kigaidi yaliyouwa watu 76 mjini Kampaka Uganda. Sasa viongozi hao wanachukua hatua madhubuti kusaidia kurejesha amani na utulivu nchini humo ikiwa ni pamoja na kuongeza vikosi vya kulinda amani Moghadishu.

Uamuzi huo unaungwa mkono na Umoja wa Mataifa ambao umekuwa msitari wa mbele pamoja na mashirika yake mbalimbali kuisaidia Somalia. Balozi Augustine Mahiga ndiye mwakilishi mpya wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akiwa kwenye mkutano huo wa AU amemfahamisha mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa Flora Nducha umuhimu wa hatua ya kuongeza vikosi Somalia.