Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza malaria ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo:Migiro

Kutokomeza malaria ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo:Migiro

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-rose Migiro amesema vita dhidi ya malaria barani Afrika kupitia ALMA vimepiga hatua.

Bi Migirio ameyasema hayo mjini Kampaka Uganda alikokuwa akihudhuria mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika AU uliomalizika leo. Bi Migiro amesema mwezi Aprili mwaka 2008 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliweka malengo ya kuhakikisha dawa za kuzuia malaria zinapatikana kwa kila muhitaji ifikapo mwisho wa mwaka huu 2010, na lengo hilo karibu linafikiwa.

Pia amemshukuru Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambaye ni kiongozi wa ALMA ambayo ni muungano wa viongozi wa Afrika katika vita dhidi ya malaria kwa jitihada zake za kuhakikisha mustakabali wa watoto wa Afrika kwa kupambana na malaria.

Amesema hatua kubwa zimepigwa na ALMA kudhibiti malaria na hasa masuala muhimu kama kuondoa kodi, katika vitu vya kuokoa maisha na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa na huduma na amesema wajibu ni wa viongozi sasa kuendeleza vita hivyo. Bi Migiro amesema kuwekeza katika kudhibiti malaria kunasaidia sio tu kuweza kufikia lengo la sita la maendeleo ya milenia bali pia la 4 na la 5 kuhusu afya ya mama na mtoto.