Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake lazima washirikishwe katika juhudi za amani Iraq:UM

Wanawake lazima washirikishwe katika juhudi za amani Iraq:UM

Kuongeza idadi ya wanawake wa Iraq katika utatuzi wa migogoro na kutafuta amani ya kudumu ni miongoni mwa mada zilizojadiliwa leo mjini Baghdad katika kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Kongamano hilo limeandaliwa katika kuadhimisha mwaka wa kumi wa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo. Kongamano hilo limewaleta pamoja maafisa wa Umoja wa Maytaifa wanaoshughulika na kupigia chepuo masuala ya wanawake, viongozi wa serikali na wabunge ili kushiriki katika siku hii ya mjadala wa wazi kuhusu wanawake na amani, ambao ni mpango wa Umoja wa Mataifa wenye lengo la kuangalia ni jinsi gani ya kuongeza idadi ya wanawake katika ushiriki wa kuimarisha amani na usalama nchini mwao.

Miongoni mwa waliozungumza kwenye kongamano hilo ni kaimu waziri wa masuala ya wanawake Khuloud Al-Majoun na mbunge Hanan Al Fatlawee ambao wamesisitiza umuhimu wa kuwa na nyenzo muhimu za kuhakikisha wanawawezesha wanawake, mfano sheria, bajeti na mafunzo hasa katika masuala ya majadiliano na maridhiano ya kitaifa.